Ntibazonkiza aigomea Yanga

Jumatano , 21st Apr , 2021

Mshambuliaji nyota wa klabu ya Yanga, Said Ntibazonkiza amezua taharuki kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo baada ya kufunga bao sekunde chache kabla mpira haujamalizika na kulazimisha afanyanyiwe mabadiliko huku akionekana kukosa furaha.

Mshambuliaji wa Yang, Said Ntibazonkiza.

Tukio hilo limetokea usiku wa jana ambapo Yanga walikuwa na mchezao dhidi ya Gwambina na mabingwa hao wakihistoria wa ligi kuu nchini walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 huku nyota huyo akifunga bao la tatu.

Samba samba na kitendo hicho, Ntibazonkiza aligongesha kidole kichwani kwake chenye maana ya kutumia akili jambo lililozua utata na kuwaacha watu njia panda wakikosa kujua tafsiri halisi kana kwamba anatumia akili ama kitendo cha kuachwa benchi halikuwa sahihi.

Ntibazonkiza alivyohojiwa na Afisa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga, Hassan Bumbuli juu ya maana ya ushangiliaji huo, Ntibazonkiza hakuwa tayari kufafanua maana yake.

“Kikubwa ni ushindi nadhani ni furaha ya sisi wote, nadhani tungezungumzia sana sana ushindi na tuzidi kumuomba mwenyeenzi Mungu atusaidie tufanye vizuri mchezo unaofuata” Ntibazonkiza alisema.

Jambo hilo lilizua hali ya kutoelewana na baadhi ya wachezaji wenzake akiwemo Deus Kaseke walioonekana kutofurahishwa na tukio hilo mpaka kudhani kuna hali ya kutoelewana kati ya wachezaji wa Yanga jambo ambalo Ntibazonkiza amelikanusha.

“Hapana, kuhusu wachezaji tupo vizuri hakuna tatizo isipokuwa muda mwingine kwenye mchezo kuna mambo mengine yanaweza yakatokea, ni pale pale kwenye mchezo yakishapita basi yanakuwa yameisha na hiyo inatokea sehemu zote ila Alhamdulilah wachezaji hatuna tatizo lolote”.

Baada ya ushindi huo, Yanga imesalia kileleni ikiwa na alama 54 baada ya kucheza michezo 26, michezo 4 nyuma na alama 2 mbele ya mabingwa watetezi Simba wanaoshika nafasi ya pili huku Azam ikiwa nafasi ya tatu kwa alama 50 na Gwambina akiwa amesalia nafasi ya 12 na alama 30.