Okwi awaaga mashabiki wa Simba, atoa ahadi

Jumatatu , 5th Aug , 2019

Mshambuliaji wa zamani wa Simba Emmanuel Okwi ambaye ni raia wa Uganda, ameiaga rasmi klabu ya soka ya Simba akiwa tayari kwenda kuanza maisha mapya ndani ya klabu ya Itthad Alex SC ya Misri na kuahidi timu hiyo itabaki moyoni mwake.

Emmanuel Okwi

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Okwi ameweka ujumbe wa kuwashukuru mashabiki kwa kumpenda na kumfanya ajisikie nyumbani kwa miaka yote ambayo amechezea klabu hiyo.

''Niwashukuru mashabiki kwa kila kitu ambacho mmenifanyia, mmekuwa watu wazuri sana kwangu, nawahakikishia kuwa upendo wenu kwangu nautambua'', ameandika Okwi.

Okwi ambaye ameichezea Simba tangu mwaka 2010, amelishukuru pia benchi la ufundi pamoja na viongozi wa Simba kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiwapa ili kufikia malengo yao binafsi na ya klabu.

''Ninawaahidi kuwa nakwenda Itthad Alex SC lakini Simba itabaki moyoni mwangu'', ameongeza.

Okwi ameichezea Simba kwa misimu isiyopungua 6 na kufunga magoli zaidi ya 70, huku akichukua makombe kadhaa ikiwemo Ligi kuu, Kombe la shirikisho nchini na mengine.