Jumamosi , 17th Nov , 2018

Mshambuliaji wa kimataifa wa klabu ya soka ya Simba kutoka nchini Uganda, Emmanuel Okwi, leo hatakuwa sehemu ya mchezo wa 5 kundi L kuwania kufuzu fainali za AFCON 2019 dhidi ya Cape Verde.

Emmanuel Okwi akiwa mazoezini na wachezaji wenzake wa Uganda.

Okwi anakosa mchezo huo kwa kuwa anatumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja kutokana na kuwa na kadi mbili za njano, hivyo atakuwa jukwaani akiwatazama wenzake.

Okwi mpaka sasa ameifungia Uganda mabao 2 kwenye michuano hiyo ya kuwania kufuzu akiwa nyuma ya Farouk Miya ambaya ana mabao matatu, huku kwa pamoja wakiisaidia timu hiyo kuaongoza kundi hilo wakiwa na alama 10.

Uganda leo inahitaji alama 1 pekee ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu fainali hizo. Mchezo huo utapigwa kuanzia saa 10:00 kwenye uwanja wa taifa wa Uganda maarufu kama Namboole.

Kundi L pia lina timu za Tanzania na Lesotho ambazo zinacheza kesho mjini Masero huko Lesotho ambapo Taifa Stars inahitaji ushindi ili kujiweka mahala pazuri kwenye mbio hizo za kwenda Cameroon.