Jumapili , 31st Dec , 2017

Baada ya kufunga mabao mawili kwenye ushindi dhidi ya klabu ya Ndanda FC mshambuliaji wa Simba John Bocco amesifiwa na wachezaji wenzake Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima.

Wachezaji hao wa kimataifa ambao wamejiunga na Simba msimu huu kama ilivyo kwa John Bocco wametumia mitandao yao ya kijamii kumpongeza nyota huyo wa zamani wa Azam FC baada ya kuiwezesha Simba kushinda na kurejea kileleni.

Okwi na Niyonzima ambao ni majeruhi wamekipongeza pia kikosi kizima cha Simba kwa kupata matokeo jana jioni kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara dhidi ya wenyeji Ndanda FC. Mabao yote yalifungwa na Bocco kipindi cha pili.

''Hongera Bocco umeongoza kwa mfano kama nahodha, hongera pia kwa wachezaji wote'', ameandika Okwi. Naye Niyonzima ameandika, ''Hongera timu nzima na kaka yangu Bocco Mungu azidi kukusimamia''.

Baada ya ushindi huo wa jana, Simba sasa imefikisha alama 26 na kukaa kileleni sawa na Azam FC, Simba ikiwa juu kwa kuwa na mabao 19 huku Azam FC ikiwa na mabao 9.