Jumatano , 19th Aug , 2020

Klabu ya Paris Saint- Germain imetinga fainali ya kwanza ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya miaka hamsini tokea kuanzishwa kwake.

Wachezaji wa PSG wakifurahia ushindi

Mafanikio hayo makubwa yamefikiwa baada ya kuichapa RB Leipzig ya nchini Ujerumani kwa mabao 3-0 usiku wa jana katika mchezo wa Nusu Fainali ya michuano hiyo nchini Ureno.

Mabao ya PSG yamefungwa na Marquinhos, Angel Di Maria na Juan Bernat na kuifanya klabu hiyo yenye mastaa ghali zaidi duniani kwa sasa, Kylian Mbappe na Neymar kutinga fainali kwa staili yake huku ikisubiri mshindi wa mechi ya Bayern Munich na Lyon itakayochezwa hii leo.

Baada ya mchezo huo, kocha wa RB Leipzig, Julian Nagelsmann (33) amesema kuwa PSG walistahili kuipata tiketi ya kufuzu hatua ya fainali kwenye mchezo huo kwa jinsi ambavyo walicheza, akisema kwamba, "ni ngumu kukubali lakini wakati mwingine ndiyo soka lilivyo".

Mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya unategemewa kuchezwa Agosti 23, 2020 nchini Ureno.