
Rais wa Shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania, Phares Magesa akizungumzia mafanikio ya ligi ya taifa ya kikapu Tanzania.
Kurasini Heat ambao ndio mabingwa wa RBA, walifanikiwa kutwaa ubingwa wa taifa ngazi ya vilabu, baada ya jana kuibuka washindi kwa alama 76- 59 dhidi ya Oilers katika fainali iliyochezwa uwanjani Don Bosco uliopo Upanga jijini Dar es salaaam.
Akizungumza na East Africa Radio Magesa amesema, ''Tunawapongeza Kurasini Heat, wamewekeza katika kila eneo ikiwemo kulipa vizuri wachezaji, walisajili vyema na wanatawala hivi sasa, kwetu Shirikisho hatusikitiki kuona timu kama Vijana, Pazi, Savio zimeshindwa, tunaona mchezo wa kikapu unakua hivyo tunajivunia''.
Kwa upande wa Kocha ambaye pia ni mmoja wa viongozi wa wa mabingwa Kurasini Heat, Shendu Mwagalla amesema waliamua kuwekeza kwa fedha zao binafsi, lengo likiwa ni kuhakikisha wanapata mafanikio ili wavutie taasisi mbalimbali ziwekezea katika mchezo wa kikapu.
''Si jambo rahisi kuendesha timu kwa fedha za watu binafsi lakini sisi tuliamua, hakuna taasisi au mfanyabiashara anayewekeza sehemu isiyo na dalili za mafanikio, hivyo tunaamini kwa kuanzia hapa tutabisha hodi sehemu mbalimbali tukiwa na mtaji na tutafanikiwa''.
Bingwa wa ligi ya taifa vilabu bingwa NBL Wanaume atawakilisha Tanzania katika mashindano ya kombe la klabu bingwa ya Afrika (Basketball Africa League - BAL) .
Licha ya kupoteza katika fainali, Oilers waliomaliza nafasi ya pili wataungana na Panthers waliomaliza kama washindi wa tatu, watawakilisha nchi katika mashindano ya vilabu ya kanda ya tano ya Afrika (Zone V Club Championship /Challenge Cup).
Panthers walimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kuifunga Vijana City Bulls kwa alama 80-77.
Kwa upande wa wanawake bingwa na mshindi wa pili wote watawakilisha katika mashindano ya vilabu ya wanawake ya kanda ya tano ya Afrika.
Jeshi Stars waliibuka mabingwa waliibuka mabingwa kwa kuwanyuka Dodoma Queens kwa alama 80- 72 huku VBQ wakimaliza nafasi ya pili.
Msimu wa ligi ya Vilabu ya Kikapu ya Tanzania ( NBL) ilianza mwezi Februari mwaka huu kwa ngazi za mikoa (RBA) na imemalizika rasmi leo 25 Oct, 2020 kwa ngazi ya Taifa.