Jumatano , 2nd Dec , 2020

Mwenyekiti wa Kamati ya Mabadiliko ya Yanga SC, Wakili Alex Mgongolwa, leo Desemba 2, 2020 amekabidhi rasmi kwa uongozi rasimu ya awali ya mfumo wa mabadiliko.

Akiongea kabla ya kukabidhi rasmi hiyo ambayo imeandaliwa kwa ushirikiano wa kamati hiyo na kamati ya La Liga pamoja na washauri mbalimbali wa ndani na nje ya Nchi, Mgongolwa amesema sasa rasmi klabu inarudi kwa wananchi.

''Tuna vipaumbele viwili kwenye rasmi yetu ya mfumo wa mabadiliko, kutakuwa na Menejimenti imara ili kuwa na taasisi bora lakini pia Wanachama wetu hatujawaacha nyuma, wao kitaalam wametambulika kama 'Fans Engagement' ambao wanatambulika rasmi na mfumo'' - Alex Mgongolwa.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Mabadiliko ya Yanga Mhandisi Hersi Said amesema, ''Leo Yanga SC tunaandika historia kwa kuleta mfumo wa uendeshaji wa klabu yetu kutoka kwenye Dunia ya kwanza kwenye soka kwa maana ya La Liga Hispania''.

Hersi ameongeza kuwa, ''Mfumo huu unakwenda kuirudisha klabu kwa wanachama na wao ndio watakuwa wamiliki halali wa klabu na baada ya mfumo kukamilika, niwahakikishie tu watu wote sio tu Tanzania bali Afrika nzima watakuja kwetu kujifunza''.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Yanga Dkt. Mshindo Msolla, amepokea rasimu hiyo na kuikabidhi kwa Mshauri wa Mabadiliko wa klabu hiyo Senzo Mbatha ili aipitie na mchakato uendelee.