Jumanne , 25th Sep , 2018

Sakata la wachezaji wa Ruvu Shooting  kuondolewa kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons linaendelea kuisumbua klabu hiyo baada ya uongozi wake kutaka TFF iwape suluhisho mbadala wachezaji wake.

Kikosi cha Ruvu Shooting.

Jumla ya wachezaji nane kati ya 18 waliosafiri na timu katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons wiki mbili zilizopita, mchezo ambao uliisha kwa sare ya kufungana mabao 2-2 ambapo wachezaji hao waliondolewa katika listi baada ya kukosa leseni kutokana na matatizo ya kimtandao kati ya TFF na FIFA.

Akizungumza na www.eatv.tv  juu ya sakata hilo na namna linavyoiathiri klabu yake, Afisa habari wa klabu ya Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema,

" Tunakutana na matatizo makubwa hivi sasa kutokana na kuwakosa wachezaji hawa, tuliingia uwanjani tukiwa na wachezaji 10 na hatukuwa na mchezaji wa akiba hata mmoja ".

" Nimeongea na katibu mkuu wa TFF, Wilfried Kidau, amenieleza jinsi wanavyohangaika kutatua changamoto hiyo na amenialika kesho niende ofisini kwake kuona namna vijana wake wanavyowasiliana na FIFA kulishughulikia tatizo hilo ili tuweze kuwatumia wachezaji wetu katika mechi ya Alhamisi ", ameongeza Masau Bwire.

Masau Bwire amesema sakata hilo limechukua muda mrefu hadi hivi sasa na kosa hilo haliko kwa wachezaji, uongozi wa klabu wala kwa shirikisho la soka Tanzania (TFF), bali liko katika masuala ya kimtandao huku akiiomba TFF kutafuta namna nyingine ya kufanya kutatua tatizo hilo na kuwaeleza namna ya kufanya endapo jitihada zitashindikana.

Ruvu Shooting itashuka dimbani Alhamisi ya wiki hii katika uwanja wake wa Mabatini itakapopambana na African Lyon katika muendelezo wa ligi kuu Tanzania bara, ambapo mpaka sasa inakamata nafasi ya 18 ya msimamo huku ikiwa na alama mbili pekee katika michezo mitano iliyocheza.