Jumatano , 8th Dec , 2021

Shirikisho la mchezo wa mpira wa kikapu nchini TBF limetoa taarifa kwa umma kuelezea sababu za timu ya Kurasini Heat kujitoa kwenye hatua ya awali ya mzunguko wapili kuwania kufuzu michuano ya klabu bingwa Afrika.

(Kikosi cha timu ya Kuraini Heat kilichocheza michezo ya kuwania BAL 2021)

Taarifa hiyo imeeleza kuwa:

“Kwa niaba ya Shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania (TBF) tunapenda kuwafahamisha kuwa timu ya kikapu ya Kurasini Heats ambao ni mabingwa wa ligi ya Kikapu Tanzania (NBL 2020) na waliwakilisha Tanzania katika mashindano ya Basketball Africa League Qualifiers (BAL 2021) yaliyofanyika Dar-es-Salaam”

“Tanzania 29-31,Oktoba, 2021 na kufuzu kwenda hatua ya pili wamejitoa katika mashindano hayo ambayo ni hatua ya mwisho (BAL Elite 16 road to BAL 2022) ambayo yanafanyika Johannesburg, Afrika Kusini 6-11 Desemba, 2021. “

“Taarifa hiyo ilitolewa na Ndg. Shendu Mwagalla kwa niaba ya Kurasini Heats ilieleza sababu za kujitoa ni kutokuwa na uhakika wa usalama wa wachezaji wao kutokana na kuibuka kwa mlipuko mwingine wa UVIKO 19 huko Afrika Kusini na ilitumwa makao makuu ya Shirikisho la mpira wa Afrika - FIBA Africa, Abidjan, Ivory Coast na TBF kupewa nakala.”

“FIBA Africa wameifahamisha TBF kuhusu uamuzi huo wa Kurasini Heats na watawasilisha taarifa hiyo ya kujitoa katika Kamati ya utendaji ya FIBA Africa ambayo ndio itatoa uamuzi wa mwisho.”

“Shirikisho la mpira wa kikapu Tanzania (TBF) linatoa wito kwa vilabu vyote vinavyoshiriki katika mashindano ya kimataifa kufanya maandalizi ya kutosha kabla ya kuthibitisha kushiriki mashindano ya kimataifa ili kuepuka usumbufu wowote unaoweza kujitokeza kwa klabu husika, TBF na FIBA”

“Tunachukua nafasi kuwashukuru wote walioshiriki Kwa namna moja ama nyingine kusaidia timu ya Kurasini Heats kushiriki mashindano haya muhimu ya klabu bingwa ya Kikapu Afrika ambayo yanaendeshwa kwa ubia kati ya FIBA Africa na chama cha mpira wa kikapu Marekani (NBA).”