Jumatatu , 6th Jun , 2016

Baada ya kukamata clip ya sauti ya baadhi ya wadau wa soka wakizungumza na kupanga mpango wa kuhujumu uchaguzi mkuu wa klabu ya soka ya Yanga hii leo ,Uongozi wa klabu hiyo umewasilisha rasmi malalamiko yao TAKUKURU ili ufanyike uchunguzi wa kina.

Mkuu wa idara ya habari wa klabu ya Yanga Jerry Muro akizungumza baada ya kutua TAKUKURU.

Uongozi wa klabu ya soka ya Yanga hii leo umefanikiwa kukabidhi barua na viambatanishi inavyoamini ni sehemu ya hujuma kwa uchaguzi wa viongozi wa klabu hiyo.

Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo , Jerry Muro amekabidhi barua na viambatanishi zikiwemo cd zenye sauti ambazo zinatuhumiwa kuwa za wadau ambao wao wanawafahamu wakizungumza na kupanga mipango ya kuhujumu uchaguzi wa klabu hiyo kwa maslai yao.

Muro alikabidhi vitu hivyo katika makao makuu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) zilizoko maeneo ya Upanga jijini Dar es Salaam.

Takukuru wameahidi kuviingiza kwenye uchunguzi na kuvifanyia kazi na watatoa taarifa uchunguzi wao pindi utakapokamilika.

Ikumbukwe uchaguzi wa Yanga utafanyika kufuatiwa na agizo la Serikali kupitia baraza la michezo nchini BMT ambalo lililiagiza shirikisho la soka nchini TFF kuhakikisha linasimamia kwa ukaribu na kuratibu uchaguzi wa klabu hiyo ambayo kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo timu hiyo haina viongozi halali wakuchaguliwa.

Lakini tangu kutolewa kwa agizo hilo na TFF kupitia kamati yake ya uchaguzi kuanzisha mchakato wake kabla ya kufanyika uchaguzi huo Juni 25 mwaka huu, ukaibuka uongozi wa Yanga ambao ulijitangaza uko kihalali kwa mujibu wa makubaliano ya moja ya mkutano mkuu wa wanachama na watamaliza muda wao baada ya uchaguzi huo ambao wameutangaza wao Yanga utakaofanyika Juni 11 mwaka huu nakukinzana na ule wa TFF uliotokana na agizo la Serikali kupitia BMT.

Mvutano huo umesababisha hata aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya TFF ambaye alipewa jukumu la kusimamia mchakato wa uchaguzi kwa niaba ya TFF Wakili Msomi Aloyce Komba kujiondoa kufuatiwa kutajwa katika watu wanaotuhumiwa kuhujumu uchaguzi huo.

Na kwa sasa tayari shirikisho la soka nchini Tanzania TFF limetangaza kutoa tamko juu ya uamuzi huo wa klabu ya Yanga kukaidi agizo la Serikali.

Wakati huo huo katika kuelekea msimu mpya wa michuano mbalimbali na dirisha kubwa la usajili kufunguliwa tayari klabu hiyo ambayo inawakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa inasemekana imeendelea kuimarisha kikosi chake mara baada ya hii leo kuwepo na taarifa kuwa klabu hiyo imemnasa kipa namba moja wa maafande wa Tanzania Prisons Benno Kakolanya.

Kipa huyo ambaye aliitwa katika kikosi cha timu ya soka ya taifa akiwa kipa namba tatu inasemekana amesaini kandarasi ya miaka miwili kuitumikia klabu hiyo ambayo tayari inamagolikipa nguli wawili Deo Munish[dida] na Ally Mustafa [Bartez] na kinda Benedict Tinnoco ambao watampa changamoto kubwa na hivyo kipa huyo pichani chini kuhitajika kujipanga.