Ijumaa , 17th Aug , 2018

Mbwana Ally Samatta, kijana ambaye alianza safari yake ya soka katika klabu ya Mbagala Market na baadae Simba kabla ya kung'aa na TP Mazembe, usiku wa Agosti 16, 2018 ameandika historia nyingine barani Ulaya baada ya kuisaidia timu yake ya KRC Genk kupiga hatua kwenye michuano ya Europa.

Mbwana Samatta kushoto akishangilia bao lake dhidi ya Lech Poznan.

Nahodha huyo wa Tanzania, ameifungia timu yake, bao la kwanza kwenye ushindi wa mabao 2-1 ikiwa ugenini dhidi ya Lech Poznan ya Poland. Mchezo huo ulikuwa ni wa marudiano Raundi ya Tatu ya mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya UEFA Europa League msimu huu.

Samatta aliitanguliza Genk dakika ya 19 tu ya mchezo kwa bao alilofunga kwa kichwa kabla ya Leandro Trossard kufunga bao la pili kwa penati dakika ya 45. Wenyeji wao Lech Poznan walifunga bao lao  dakika ya 50 kupitia kwa Tomasz Cywka.

Huu ni mwendelezo wa mwanzo mzuri wa Samatta kwenye raundi za mapema za Europa League baada ya kufungua akaunti ya mabao kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Lech Poznan mjini Genk ambapo alifunga dakika ya 56.

Kwa matokeo hayo, Genk sasa wamefuzu hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi, ambako watacheza mechi moja zaidi nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ataingia hatua hiyo.