Jumanne , 17th Mei , 2016

Timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania Serengeti Boys wamewaonyesha soka wenyeji wao timu ya India kwa kuwachapa magoli 3-1 katika mechi ya michuano ya vijana ya AIFF inayoendelea Mjini Goa.

Serengeti Boys walioonyesha soka safi ambapo katika dakika ya 20 ya mchezo walifanikiwa kupata goli kupitia kwa Maziku Amani huku dakika ya 28 Maziku tena aliweza kufumania nyavu tena na kuipatia Serengeti boys goli la pili.

Baadaye India walionekana kuamka na kufanikiwa kupata goli katika dakika ya 36 kupitia mchezaji wao Komal Thatal na hadi mapumziko matokeo yakawa ni Tanzania 2-1 India.

Kipindi cha pili, vijana hao wa Tanzania ndiyo walionyesha soka bomba zaidi na kufanikiwa kupata goli jingine la tatu katika dakika ya 47, mfungaji akiwa Asad Ali.

Baada ya hapo, Serengeti Boys walionekana kuuchezea zaidi mpira, wakipiga pasi za uhakika na kuwakatisha tamaa kabisa wenyeji hao ambao kikosi chao kilichotengenezwa chini ya uangalizi bora kwa zaidi ya miaka mitano.

Baada ya mchezo huo Serengeti Boys inaongoza na inasubiri mchezo mwingine utakaopigwa Alhamis Mei 19 dhidi ya Korea Kusini ambayo inashuka kucheza mchezo wake wa kwanza usiku wa leo dhidi ya Malaysia.