Jumanne , 14th Apr , 2015

Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji ya Bodi ya Ligi imempiga faini ya Sh 500,000 na kumfungia mechi tatu Kocha wa Kagera Sugar, Jackson Mayanja kwa kutoa lugha ya kashfa na vitendo kwa waamuzi wa mechi yao na Mtibwa Sugar kuwa walipewa rushwa.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Afisa habari wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Baraka Kizuguto amesema, adhabu dhidi ya Kocha Mayanja kwenye mechi hiyo namba 136 iliyochezwa Aprili 1mwaka huu Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya Ligi Kuu.

Kizuguto amesema adhabu hiyo pia imeikuta Klabu ya Simba ambayo imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa mujibu wa kanuni baada ya timu hiyo kugoma kuingia kwenye vyumba vya kuvalia nguo kwenye uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga wakati wa mechi dhidi ya Kagera Sugar ambapo hatua hiyo ilisababisha wachezaji wakaguliwe kwenye gari lao ambapo Klabu hiyo imepigwa faini ya sh. 500,000 tena baada ya kugoma kuingia vyumbani wakati wa mapumziko kwenye mechi hiyo hiyo.

Kizuguto amesema, kwa upande wa Klabu ya Mtibwa Sugar nayo imepigwa faini ya sh. 500,000 baada ya timu hiyo kukataa kuingia vyumbani wakati wa mapumziko katika mechi namba 142 dhidi ya Stand United iliyochezwa Aprili 5 mwaka huu, Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Kizuguto amesema, Kipa Tony Kavishe wa Polisi Morogoro amepigwa faini ya sh. 500,000 na kufungiwa mechi tatu kwa kosa la kumpiga ngumi mwamuzi msaidizi namba mbili, Hassan Zani kwa kuzingatia kanuni ya 37(5) ya Ligi Kuu. Alifanya kosa hilo kwenye mechi namba 147 dhidi ya Mgambo Shooting iliyochezwa Aprili 5, 2015 katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.