Jumatatu , 13th Aug , 2018

Kikosi cha klabu ya soka ya Simba ambacho kimefika jana jijini Dar es salaam kikitokea mkoani Lindi ambako kilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Namungo FC, leo kinaelekea mkoani Arusha kuendelea na kambi ya maandalizi ya msimu ujao.

Wachezaji wa Simba

Idara ya mawasiliano ya klabu hiyo imeweka wazi hilo kwa kueleza kuwa kikosi hicho kimefanya mazoezi ya leo asubuhi Agosti 13, 2018, kwenye viwanja vya Gymkhana ikiwa ni sehemu ya kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii pamoja na kuanza kwa ligi kuu Tanzania Bara. 

''Baada ya mazoezi ya leo kikosi cha Simba leo kinatarajia kusafiri kuelekea mkoani Arusha ambapo kinatarajia kucheza mchezo mmoja wa kirafiki na timu ambayo tutaiweka wazi kabla ya kuelekea jijini Mwanza kwaajili ya mchezo wa Ngao ya jamii Agosti 18'', imeeleza taarifa hiyo.

Hata hivyo Simba bado haijaweka wazi juu ya hali ya nahodha wao John Bocco ambaye amekosa mechi zao zote za kirafiki kutokana na kusumbuliwa na majeruhi. Katika msimu wa 2018/19 Simba itashiriki kwenye michuano mitatu tofauti ambayo ni Ligi kuu, kombe la shirikisho nchini na klabu bingwa Afrika.