Jumapili , 2nd Apr , 2017

Wachezaji wawili ambao wamewahi kuitumikia Simba SC, wametosha kuipa ushindi wa mabao 2-1 Kagera Sugar na kuwazamisha mabosi wao wa zamani katika mchezo wa ligi kuu Tanzania bara uliopigwa leo katika dimba la Kaitaba, Mjini Bukoba

Kagera Suga wakishangilia bao, wa kwanza kulia na Mbaraka Yusuph, mfungaji wa bao la kwanza

Wachezaji hao ni Mbaraka Yusuph aliyepachika bao la kwanza katika dakika ya 28 ya mchezo kwa shuti kali la umbali mrefu nje ya box baada ya mabeki wa Simba kushindwa kukaba na kumfanya kinda huyo wa Taifa Stars kumchungulia kipa wa Simba Daniel Agyei ambaye alikuwa mbali kidogo ya lango, na kuuzamisha mpira wavuni.

Hilo ni bao la 11 kwa Mbaraka Yusuph msimu huu akiwa sawa na Shiza Kichuya, nyuma ya Saimon Msuva

Mchezaji mwingine ni Edward Christopher ambaye amemalizia vizuri kros ya Suleiman Mangoma kutoka upande wa kulia baada ya Jonas Mkude kuporwa mpira huku mabeki wa kati Abdi Banda na Juuko Murshid wakikosa mawasiliano na kujikuta wakimuacha Edo akiwa peke yake ndani ya box, na kuiandikia Kagera Sugar bao la pili dakika ya 46, ikiwa ni sekunde chache tangu kuanza kwa kipindi cha pili.

Wachezaji wa Kagera Sugar baada ya mchezo

Simba ambao walimiliki zaidi mpira, walianza mchezo wa leo kwa kasi na kupoteza nafasi mbili kupitia mashuti makali ya Said Ndemla mwanzoni mwa mchezo, lakini pia iliweza kutengeneza nafasi nyingine kadhaa lakini uimara wa golikipa wa Kagera Sugar ambaye amewahi kuwa nahodha wa Simba, Juma Kaseja uliinyima kabisa Simba nafasi ya bao.

Dakika ya 61 ya mchezo baada ya kuingia kwa Juma Luizio kuchukua nafasi ya Ibrahim Ajibu, Mzamiru Yassin aliipatia Simba bao la kufutia machozi baada ya kumalizia mpira uliotemwa na kipa wa Kagera Juma Kaseja kufuatia shuti kali la Juma Luizio.

Juma Kaseja

Hadi mwisho wa mchezo, Simba imetoka dimbani ikiwa imelowa kwa kipigo cha mabao 2-1, ukiwa ni mchezo wake wa nne kupoteza katika msimu huu, na kumfanya Yanga aendelee kula raha kileleni ikiwa na pointi 56 huku Simba wakibaki na point zao 55.

Ushindi huo umeisogeza Kagera Suga hadi nafasi ya 3 ikiwa na point 45, ikiipiku Azam yenye point 44 katika nafasi ya 4

Baada ya mchezo huo Simba inakwenda mwanza kwa ajili ya michezo miwili kati ya Mbao FC na Toto Africans.

Majimaji nayo imeipiga Toto African mabao 4-1, African Lyon imeifunga Stand United bao 1-0 na Mtibwa imecheza na Tanzania Prisons na kutoka suluhu