Jumamosi , 15th Aug , 2020

Klabu ya Simba ya Jijini Dar es salaam imeendeleza kutambulisha usajili wa wachezaji wake wapya ambapo jioni ya leo imemtangaza Larry Bwalya kutoka Zambia aliyesaini mkataba wa miaka miwili.

Nyota mpya wa Simba, Larry Bwalya (Kulia Pichani) akisaini mkataba akiwa na Kocha msaidizi wa wekundu hao wa Msimbazi Seleman Matola (Kushoto).

Kupitia mitandao yake ya kijamii, Simba imetoa taarifa ya kumsani nyota hiyo mwenye umri wa miaka 25 ambaye alikua akiichezea Zanaco ya Nchini Zambia.

Awali iliripotiwa kuwa kiungo huyo mahiri alifanya mazungumzo na Klabu ya soka ya Yanga lakini ghafla mipango hiyo ikafutika na ni rasmi hivi sasa nyota huyo ni mali ya Simba.

Bwalya anaungana na Joash Onyango raia wa Kenya ambaye hapo jana alitambulishwa rasmi kujiunga na miamba hiyo ya soka hapa nchini.

Vilevile Simba leo imemtambulisha David Kameta ambaye ni beki wa kulia aliyetokea katika Klabu ya Lipuli ambayo ilishuka daraja.

Wachezaji wengine ambao wameshasajiliwa na Simba ni pamoja na Benard Morrison aliyetoka Yanga na  Charles Ilamfia aliyetokea KMC.