Simba yagawa kichapo kwa Waarabu

Jumamosi , 12th Jan , 2019

Klabu ya soka ya Simba imefanikiwa kuibuka na ushindi katika mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi Klabu Bingwa Barani Afrika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mohammed Dewji wakiwa uwanjani.

Mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa umeshuhudia Simba ikiichapa JS Saoura ya Algeria kwa mabao 3-0 na kujikusanyia pointi tatu zinazowaweka juu ya kundi lao lenye timu nne.

Mabao ya Simba yamepachikwa kimiani na Emmanuel Okwi katika dakika ya 45+2 huku bao la pili na la tatu yakifungwa na mshambuliaji Meddie Kagere katika dakika ya 51 na 67, na kushuhudia shangwe kubwa msimbazi.

Mchezo huo pia ulihudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye asubuhi alikuwa Kisiwani Pemba katika sherehe za maadhimisho ya 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar, lakini hakukubali kupitwa baada ya kuunganisha moja kwa moja uwanjani hapo.

Pia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikuwa sambamba na mwekezaji wa klabu hiyo, bilionea Mohammed Dewji 'Mo' pamoja na mgeni rasmi, ambaye ni Naibu Spika, Tulia Ackson.

Simba inashiriki hatua ya makundi kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2003 na hatua kubwa zaidi iliyowahi kufikia katika michuano ya Klabu Bingwa Barani Afrika ni hatua ya fainali mwaka 1993 ambapo ilipoteza dhidi ya Stella Adjamé ya Ivory Coast.