Ijumaa , 29th Jan , 2021

Klabu ya Simba imemtoa kwa mkopo mshambuliaji wake, Charles Ilanfya kurudi kwenye klabu yake ya zamani ya KMC kwa kandarasi ya miezi sita itakayomalizika mwishoni mwa msimu huu.

Charles Ilanfya akifanya mazoezi alipokuwa na kikosi cha Simba.

Tokea Ilanfya ajiunge na Simba kipindi cha dirisha kubwa la usajili la mwaka jana akitokea KMC, amekosa nafasi kwenya kikosi cha kwanza kufuatia ushindani mkubwa wa nafasi uliopo kikosini hapo licha ya usajili wake kuwa chaguo la mwalimuSven Vanderbroeck.

Ilanfya ameshindwa kupata nafasi mbele ya washambuliaji, nahodha John Bocco, Meddie Kagere na Chris Mugalu ambao wameonesha uwezo mkubwa sana wa kufumania nyavu huku Ilanfya akifunga bao moja pekee dhidi ya klabu ya Biashara United Mara kwenye VPL.

KMC pia imethibitisha kumnasa aliyekuwa mshambuliaji wa klabu ya Yanga, Matteo Anthony kutoka klabu ya KMKM ya visiwani Zanzibar kwa kandarasi ya mwaka mmoja na nusu kuwatumikia vijana hao wa kinondoni.

Usajili wa washambuliaji hao umefanywa ili kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na mshambuliaji Reliant Luisajo aliyetoka KMC na kutimkia klabu yake ya zamani ya Namungo ya mkoani Lindi.