Haji Manara
6. Ni idadi ya kadi nyekundu zilizotolewa kwenye michuano ya Euro 2020 mpaka sasa, wakati tukiwa tunaelekea kwenye michezo ya hatua ya Nusu faini ya michuano hiyo.
Wachezaji walionyeshwa kadi hizo ni Remo Freuler wa Uswiss, Grzegorz Krychowiak wa Poland, Enthan Ampadu na Harry Wilson wa Wales, Matthijs de Ligt wa Uholanzi na Marcus Danielson wa Sweden.
5. Ni jumla ya mataji ya Wimbledon aliyoshinda Novak Djokovic ambaye ndio bingwa mtetezi wa michuano hiyo ya tenisi, ambapo amefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya kumfunga Cristian Garin wa italia kwa seti tatu mfululizo kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora uliochezwa kwa Saa 1 na dakika 49.
Djkovic raia wa Serbia ametinga hatua ya robo fainali kwa mara ya 12 kwenye Wimbledon na ya 50 kwenye michuano ya Grandslams na katika hatua hiyo atacheza dhidi ya Marton Fucsovics wa Hungary.
4. Ni idadi ya siku za mapumziko ambazo walipewa wachezaji wa Yanga baada ya kuibika na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya watani zao Simba Sc kwenye mchezo wa Dabi ya Kariakoo siku ya Jumamosi, na sasa kikosi hicho kitarejea tena kambini Siku ya Jumatano na kuanza maandizi ya kujiandaa na michezo ya Ligi Kuu inayofata dhidi ya Ihefu na Dodoma Jiji. Yanga ina alama 70 na inashika nafasi ya pili kwenye msimamo.
3. Ni sawa na michezo iliyofungwa klabu ya Simba SC kwenye michezo ya ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu, na mara baada ya kupoteza mchezo wa 3 msimu huu siku ya Jumamosi dhidi ya watani zao Yanga kwa bao 1-0, hapo jana msemaji wa klabu hiyo Haji Manara ameandika kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram kuwa ataacha kazi endapo kama timu hiyo itafungwa tena na Yanga kwenye mchezo wa fainali ya kombe la Azam Sports Federation Cup.
Simba na Yanga zitakutana katika mchezo wa fainali ya michuano hiyo Julai 25 mchezo utakao chezwa katika dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
2. Ni idadi ya michezo iliyoshinda timu ya taifa ya Italia dhidi ya Hispania kwenye michezo 14 ya mwisho timu hizo kukutana. Ambapo Timu hizi zitashuka Dimbani leo Usiku kuminyana kwenye mchezo wa Nusu fainali ya michuano ya Euro 2020 mchezo utakao chezwa Saa 4:00 Usiku.
Mara ya mwisho timu hizi kukutana kwenye michuano ya Euro ilikuwa Kwenye Euro 2016 hatua ya 16 bora na Italia ilishinda kwa mabao 2-0 ambayo yalifungwa na Giorgio Chiellini na Graziano Pelle.
1. Ni bao pekee lilofungwa kwenye mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Copa, ambapo Brazil imeibula na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Peru bao lilofungwa na Lucas Paqueta akiitumia vyema pasi ya Neymar Jr.
Brazil ambao ni mabingwa mara 9 wa michuano hii na ndio mabingwa watetezi wamefuzu kucheza fainali kwa mara ya 21, na sasa watacheza fainali na mshindi wa nusu fainali ya pili itakayo zikutanisha timu za Argentina na Colombia.





