Jumatano , 17th Apr , 2019

Mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa Ulaya kati ya Manchester City na Tottenham Hotspurs unatarajia kupigwa hii leo katika dimba Etihad.

Mchezo wa kwanza wa Klabu Bingwa Ulaya, Tottenham Hotspurs na Man City

Katika mchezo wa kwanza, Tottenham Hotspurs iliibuka na ushindi wa bao 1-0 katika uwanja wake mpya wa nyumbani, bao pekee lililofungwa na Heung-min Son katika kipindi cha pili.

Timu hizo pia zina mchezo mwingine wa Ligi Kuu nchini Uingereza EPL wikiendi hii, hali hiyo inayozidi kuifanya mechi kuwa ni ya kuvutia zaidi ambapo Man City inahitaji ushindi pekee ili iweze kuweka hai matumaini ya kuufukuzia ubingwa wa EPL, huku Spurs ikihitaji pia alama tatu ili iendelee kubakiza matumaini ya kubakia 'Top Four'.

Ili kuweza kuhakikisha inafanya vizuri, Spurs inahitaji kuchagua mashindano ya kuwekea nguvu zaidi kati ya Klabu Bingwa Ulaya au EPL kwa sababu katika ligi inakamata nafasi ya tatu ikiwa na pointi 67, mbele kwa nafasi moja dhidi ya Arsenal iliyo katika nafasi ya nne kwa pointi 66.

Endapo itaamua kuwekeza nguvu katika Klabu Bingwa, inahitaji kupanga kikosi kazi cha nguvu dhidi ya City ili iweze kuwaondoa na kutinga hatua ya nusu fainali, na kama itahitaji zaidi kumaliza nafasi nne za ligi ili waweze kurudi katika michuano ya Ulaya, basi inahitaji kuwekeza nguvu zaidi katika mchezo wa wikiendi.

Kutokana na ubora wa vikosi vyote viwili, Manchester City ndiyo inayopewa nafasi kubwa zaidi ya kufanya vizuri katika michezo yote miwili kutokana na wachezaji wake wote muhimu kuwa fiti tofauti na Spurs ambayo tayari imeshapata jeraha la kuondokewa na mshambuliaji Harry Kane ambaye atakuwa nje ya uwanja hadi mwisho wa msimu.