Jumatatu , 25th Jan , 2021

‘Masharobaro wa jiji la London’, Klabu ya Tottenham Hotspurs huenda ikawakosa nyota wake watatu kwenye mchezo wa mzunguko wa nne wa kombe la FA nchini Uingereza watakaocheza dhidi ya Wycombe Wanderers saa 4:45 usiku wa leo tarehe 25 Januari 2021.

Mlinzi wa kulia wa Spurs, Sergie Aurier (kushoto) akishangilia bao na Delle Ali (kushoto).

Wachezaji waliopo kwenye mashaka ya kukosekana kwenye mchezo huo ni kiungo mshambuliaji Dele Alli na walinzi wa kulia wawili, Serge Aurier na Matt Doherty ambao wanasubiri majibu ya vipimo vya mwisho kutoka jopo la madaktari yatakayotoka jioni ya leo.

Licha ya nyota hao watatu kuwa kwenye mashaka ya kucheza, kocha wa Spurs, Jose Mourinho amethitibisha kiungo wake Giovani Lo Celso ataendelea kukosekana kutokana na majeraha lakini Gareth Bale na Vinicious huenda wakaanza kwenye kikosi cha kwanza.

(Mshambuliaji wa Spurs, Gareth Bale)

Kutokana na maneno hayo ya Mourinho ni dhahili shahiri atawaanzisha benchini washambuliaji wake tegemezi, nahodha Harry Kane na Son Hueng-Min ikiwa ni mahesabu ya kuwawinda Liverpool kwenye EPL mchezo utakaochezwa tarehe 28 Januari 2021.

Spurs ambayo haijafungwa kwenye michezo yake saba ya mwisho tokea disemba 20 ilipofungwa 2-0 na Leicester City, ikipata ushindi kwenye mchezo wa leo basi itatinga hatua ya mzunguko wa tano na kufukuzia kutinga fainali ya pili baada ya kutinga ya Carabao Cup.

Kwa upande wa Wycombe Wanderers, watamkosa mlinzi wake mkongwe Anhony Stewart kutokana na majeraha na kutegemea nyota wake wawili Daryl Horgan na Scott Kashket kurejea kikosini kupambana na vijana hao wa Jose Mourinho.

Mara ya mwisho Spurs kukutana na Wycombe Wanderers kwenye michuano hii ilikuwa ni mwaka 2017 ambapo Spurs walipata ushindi wa mabao 4-3 kwenye dimba la White Hart lane na mabao mawili ya kuinusuru Spurs dakika za mwisho yalifungwa na Delle Alli na Son Hueng-Min.