Jumatatu , 18th Jan , 2021

Ligi kuu nchini England inatazamiwa kuendelea usiku wa leo tarehe 18 Januari 2021 kwa mchezo mmoja, 'Washika mitutu wa jiji la London' klabu ya Arsenal itawakaribisha Newcastle United inayonolewa na kocha Steve Bruce mchezo utakaochezwa sa 4:00 usiku leo kwenye dimba la Emirates.

Kocha wa klabu ya Newcastle United, Steve Bruce.

Kuelekea kwenye mchezo huo, Arsenal itamkosa mlinzi wake wa kati Pablo Mari ambaye anasumbuliwa na maumivu ya misuli ya nyuma ya goti aliyoyapata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Crystal Palace na kumfanya afanyiwe mabadiliko baada ya maumivu kumzidia.

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema kuna hati hati kama mlinzi wake wa kushoto Kieran Tierney anayesumbuliwa na maumivu ya misuli na mshambuliaji wake Gabriel Martinelli mwenye maumivu kwenye kifundo chake cha mguu kama wataweza kucheza kwenye mchezo huo.

Taarifa nzuri kwa washika mitutu hao wa jiji la London ni kwamba, kiungo wake mpya Thomas Partey aliyesajiliwa dirisha kubwa la usajili lililopita anatazamiwa kurejea dimbani baada ya kupona maumivu  kwenye kifundo chake cha mguu na mlinzi Gabriel Magalhaes kuripitiwa kuwa fiti kuwavaa Newcastle

Kwa upande Newcastle United inayonolewa na kocha Steve Bruce, itamkosa winga wake Ryan Fraser anayetumikia aadhabu ya kukosa mchezo mmoja baada ya kuoneshwa kadi mbili za njano kwenye mchezo uliopita na kiungo Jonjo Shevley atakosekana baada ya kufanyiwa upasuaji wa paja.

Walinzi wa kati na nahodha wa Newcastle Jamal Lascelles na nahodha msaidizi Federico Fernandez hawana uhakika wa kuwemo kikosini baada ya kukutwa na Covid-19 hivyo watasubiri majibu ya vipimo vya mwisho kuonesha kama wapo fiti ama laa.

(Kwenye picha: Ni kiungo mshambuliaji wa Arsenal, Eddie Smith Rowe akipiga mpira na kuifungia Arsenal bao la pili kwenye ushindi wa Arsenal wa mabao 2-0 dhidi ya Newcastle kwenye kombe la FA siku tisa zilizopita.)

Mchezo huo ni fumbo kwa kocha wa Newcastle United Steve Bruce kutokana na rekodi yake mbaya mbele ya Arsenal kwenye dimba la Emirates ambapo amecheza michezo 11 dhidi ya Arsenal na kufungwa michezo 8 na kuambuliwa sare tatu bili ushindi akiwa ugenini dhidi ya Arsenal.

Leo wafuatiliaji wa soka Ulimwenguni watasubiri kuona kama kocha huyo atavunja uteja akiwa ugenini mbele ya Arsenal baada ya mchezo kumalizika. Kwa upande wa Arsenal na wenyewe hawana rekodi nzuri kwenye dimba lao hilo msimuu, wamecheza michezo 8 lakini wameshinda mchezo 1 tu.

Kwa rekodi hiyo, maana yake Arsenal wameambulia alama 5 kati ya 21 zilizotarajiwa kama wangepata ushindi kwenye michezo 7 waliyocheza na badala yake kushinda mchezo 1 pekee, kutoa sare 2 na kufungwa michezo 4 kwenye dimba la Emirates kwenye EPL msimu huu.

Arsenal ambaye wameifunga Newcastle mabao 2-0 siku 9 zilizopita na kuwatoa kwenye mzunguko wa tatu wa kombe la FA, huenda wakiingia kifua mbele na rekodi yao nzuri mbele ya Newcastle ya kuwafunga mara 14 kwenye michezo 15 ya mwisho waliyocheza tokea wafungwe 2010 bao 1-0.