Alhamisi , 1st Jan , 2015

Shirikisho la Mpira wa Wavu Afrika CAVB, limeichagua Tanzania kuwa wenyeji wa michuano ya Kanda ya Tano ya Mpira wa Wavu wa Ufukweni inayotarajiwa kufanyika Februari 16 mpaka 18.

Akizungumza na East Africa Radio, Mkurugenzi wa Kamisheni ya mchezo wa wavu wa ufukweni, Muharrami Mchume amesema michuano hiyo ambayo ni sehemu ya kufuzu kwa michuano ya Olimpiki itakayofanyika Rio de Janeiro, Brazil mwaka 2016 inatarajia kushirikisha nchi za Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia, Djibouti na wenyeji Tanzania.

Mchume amesema, hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa wenyeji wa michuano hiyo ambapo CAVB ipo katika jitihada za kuendeleza mchezo huo wa ufukweni ambapo hivi karibuni liliendesha semina nchini Tanzania ambayo ilishirikisha washiriki kutoka zaidi ya nchi Tano katika jitihada za kuukuza mchezo huo katika nchi za kanda ya Tano hasa mashuleni.