Jumatano , 3rd Feb , 2021

Timu ya taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20, Ngarongoro Heroes, itashuka dimbani leo usiku kuminyana na timu ya taifa ya Uganda ya umri huo.

Tanzania na Uganda ndio wawakilishi kutoka ukanda wa CECAFA kwenye michuano ya soka barani Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20

Huu ni mchezo wa kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi kueleka katika michuano ya AFCON kwa wachezaji chini ya miaka 20, itakayofanyika Mauritania.

Timu zote hizi zimefuzu kucheza fainali za michuano ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 AFCON, na ndio wawakilisha kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na kati (CECAFA), fainali ambazo zitaanza kutimua vumbi Februari 14 nchini Mauritania.

Mchezo huu ni sehemu ya michezo miwili itakayozikutanisha timu hizi ambayo ni ya kirafiki, ikiwa ni michezo maalumu kwa timu hizi kabla ya fainali hizo, mara ya mwisho timu hizi kukutana ilikuwa katika mchezo wa fainali wa michuano ya vijana chini ya umri huo kutoka ukanda huu wa CECAFA, ambapo Tanzania ulifungwa mabao 4-1.

Kwenye michuano ya AFCON Tanzania imepangwa kundi C, sambamba na mataifa ya Ghana, Gambia na Morocco. Wakati Uganda wamepangwa kundi A pamoja na wenyeji Mauritania, Cameroon na Msumbiji.

Mchezo wa pili utachezwa Februari 6, katika dimba hilo hilo la Azam Complex.