Ijumaa , 1st Jul , 2022

Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’ limethibitisha kuwa litatuma teknolojia mpya yenye utaalam wa hali ya juu ya kutambua mchezaji atakayeotea ‘Offside’ kwenye michuano ya kombe la Dunia inayotaraji kuanza Novemba 21, 2022 Nchini Qatar.

Gianni Infantino - Rais wa FIFA

Teknolojia hiyo itahusisa uwepo wa ‘sensor’ yaani kifaa maalumu cha kuhisi kitu kitakachowekwa ndani ya mpira huku kikiwa na uwezo wa kutuma taarifa mara 500 kwa sekunde kwa kusoma uelekeo halisi wa mpira.

Mbali na ‘Sensor’, lakini kutakuwa na kamera maalumu 12 ambazo zitawekwa kwenye kila paa la uwanja kwa ajili ya kufuatilia mwendo wa kutoka kwenye mwili wa kila mchezaji kwa kutuma taarifa mara 50 kwa sekunde kwa mchezaji aliye na mpira kwa wakati husika.

Mchezaji yeyote akiwa kwenye nafasi ya kuotea ‘Offside’ taarifa ya tahadhari itatumwa katika chumba cha waamuzi wasaidizi kwa njia ya video ambapo waamuzi hao watatuma taarifa haraka kwa mwamuzi wa kati ili imsaidie afanye maamuzi.

Mfumo huo ulijaribiwa katika michezo ya kombe la Dunia la vilabu msimu wa mwaka jana ambapo ilikadiriwa kupunguza muda uliokuwa unatumiwa na VAR kufanya maamuzi ya ‘Offside’ kutoka sekunde 70 hadi sekunde 25.

Upande wa mkuu wa waamuzi wa FIFA, Pierluigi Collina alisema mfumo huo ni mzuri na sasa uko tayari kwa ajili ya kutumika na waamuzi. Michuano hiyo mikubwa ya soka Duniani itaraji kuanza 21 Novemba 2022 na kutamatika Desemba 18, 2022 nchini Qatar.