Ijumaa , 8th Dec , 2017

Mchezaji wa timu ya Singida United ya Singida, Mudathir Yahaya amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa ligi kuu soka Tanzania Bara (VPL) kwa mwezi Novemba.

Mudathir ametwaa tuzo hiyo baada ya kumshinda mchezaji mwenzake wa Singida United mshambuliaji Danny Usengimana pamoja na beki wa Lipuli FC ya Iringa Asante Kwasi. Mudathir aliingia fainali ya kuwania tuzo hiyo ya mwezi Novemba msimu wa 2017/2018.

Kiungo huyo amepata tuzo hiyo baada ya mapendekezo kutoka kwa makocha na uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii kwenye kikao cha Kamati ya Tuzo za VPL zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mchezaji huyo alitoa mchango mkubwa kwa Singida United mwezi huo ikipata pointi saba katika michezo mitatu iliyocheza na kupanda katika msimamo wa ligi kutoka nafasi ya sita iliyokuwepo mwezi Oktoba hadi ya nne.

Singida United ilitoka 0-0 na Yanga, iliifunga Mbeya City mabao 2-1 na pia iliifunga Lipuli bao 1-0, ambapo Mudathir anayecheza nafasi ya kiungo alicheza dakika zote 270 sawa na michezo mitatu na hakuwa na kadi yoyote.

Mafanikio hayo yamemsaidia Mudathir kurudishwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na ile ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, ambayo inashiriki michuano ya CECAFA Senior Challenge inayoendelea nchini Kenya.