Jumatatu , 6th Jun , 2016

Klabu za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara zimetakiwa kuanzia msimu ujao ziwe na ofisi, uwanja wa mazoezi, kuendeleza programu za vijana ikiwa ni pamoja na kuwapa haki ya kusoma.

Hayo yamefikiwa hapo jana Juni 05 2016 mwaka huu katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) cha kupitia taarifa mbalimbali za ligi na kukubaliana namna ya kuboresha mashindano mbalimbali ikiwamo Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza, Ligi Daraja la Pili na Ligi ya Mabingwa wa Mkoa kilichofanyika mjini Dar es Salaam.

Kamati pia iliangalia uendeshaji wa Ligi za vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 na Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL).Pamoja na hayo, Kamati ya Utendaji imepitisha azimio la kanuni ya leseni ya klabu kuwa ni lazima ianze kutumika msimu mpya wa mashindano wa 2016/17.

Mahitaji ya kanuni hiyo ni pamoja na klabu kuwa na Watendaji wa kuajiriwa kama vile Katibu Mkuu (GS), Mkurugenzi wa Ufundi (TD), Ofisa Usalama (Security Officer) na taarifa ya fedha zilizokaguliwa pamoja na Meneja wa Fedha ambaye atakuwa na uwezo wa kuandaa taarifa za fedha zitakazokaguliwa na wakaguzi wa mahesabu.

Kamati imevitaka vilabu pia kuwa na ofisi, uwanja wa mazoezi, kuendeleza programu ya vijana ikiwa ni pamoja na kuwapa haki ya kusoma na kwamba hakuna mmiliki mmoja anayeruhusiwa kuwa na timu zaidi ya moja katika ligi.