Jumanne , 17th Jul , 2018

Timu ya mpira wa Kikapu ya Team Kiza, wameipongeza kamati ya maandalizi ya michuano ya Sprite Bball Kings kwa kuipeleka michezo ya robo fainali kwenye uwanja wa ndani wa taifa kwani ndio uwanja ambao wanauzoefu nao.

Wachezaji wa Team kiza waliovaa jezi za blue kwenye mechi yao ya 16 bora dhidi ya Ukonga Warriors waliovaa nyeupe.

Akiongea na www.eatv.tv  nahodha wa timu hiyo Magige Thomas, amesema kitendo cha kamati kupeleka mechi za robo fainali kwenye uwanja wa ndani wa taifa kimewafurahisha kwani wachezaji wengi wa timu yao ni wazoefu wa uwanja huo.

''Kwanza tunawapongeza waandaaji (East Africa Television) kwa kupanga robo fainali ichezwe uwanjwa wa ndani, wapinzani wetu ambao ni DMI wajiandae wakijua wana kazi sana maana ule uwanja sisi tunaujua kwahiyo tutakuwa kama tupo nyumbani tu'', - amesema.

Mashindano ya Sprite Bball Kings yanayodhaminiwa na kinywaji cha Sprite yapo katika hatua ya robo fainali na mechi nne za hatua hiyo zitapigwa Jumamosi Julai 21 kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 2:00 usiku.

Mechi za robo fainali ambazo zitaamua timu 4 zinazoelekea nusu fainali na baadae fainali kuzisaka zile milioni 10 kwa bingwa, milioni 3 mshindi wa pili na milioni 2 kwa MVP ni Temeke Heroes Vs Portland, Mchenga Bball Stars Vs St. Joseph, Team Kiza Vs DMI na Water Institute  Vs Flying Dribblers.