Alhamisi , 7th Oct , 2021

Mabingwa wa michuano ya EURO 2021, Timu ya taifa ya Italia imeshindwa kutinga fainali ya michuano ya Uefa Nations League ‘UNL’ baada ya kufungwa 2-1 na timu ya taifa ya Uhispania kwenye mchezo uliocheza usiku wa kuamkia leo Oktoba 7, 2021 kwenye dimba la San Siro.

(Wachezaji wa timu ya taifa ya Uhispania, wakisheherekea na kumpongeza Ferran Torres kwa kufunga bao dhidi ya Italia usiku wa Jana.)

Mabao ya Uhispania yamewekwa kimiani na mshambuliaji wake Ferran Torres dakika ya 17 na 45 kabla ya kwenda mapumziko huku ikishuhudiwa nahodha wa mchezo huo beki Leonardo Bonucci akioneshwa kadi nyekundu dakika ya 42 kabla ya Lorenzo Pellegrini kufunga bao dakika 83 la kufutia machozi kwa Italia.

Kipigo hiko kimewafanya Uhispania kuvunja rekodi ya Italia ya kucheza michezo 37 mfululizo ya michuano yote bila kufungwa mwaka 2018, rekodi ambayo bado imeshikilia kuwa rekodi ya muda mrefu kwa timu za taifa za wanaume Duniani.

Pia, Italia imefungwa kwa mara ya kwanza kwenye mchezo rasmi kwenye uwanja wake wa nyumbani tokea mwaka 1999 wakati ambao wachezaji makinda wa Uhispania sita waliokuwa kwenye mchezo wa jana waliokuwa hawajazaliwa ambao ni Pedro Porro, Ferran Torres, Eric Garcia, Bryan Gil, Yeremia Pino na Gavira ‘Gavi’.

Kwa upande mwingine, Uhispania imezidi kuonesha ubabe wake mbele ya Italia, kwani ilikuwa ni mchezo wao wa 34, Hispania wakishinda michezo 12, Italyakishinda 10 na wakitoa sare mara 12.

Mchezo wa nusu fainali ya pili ya michuano hiyo, itachezwa saa 3:45 usiku wa leo Oktoba 7, 2021 kwenye dimba la Allianz Arena ambapo Ubelgiji watakipiga na Ufaransa na fainali itachezwa Jumapili ya Oktoba 10, 2021 kwenye dimba la San Siro nchini Italia.