Ijumaa , 31st Jul , 2020

Jana Julai 30, 2020 ilitoka taarifa kuwa Rais wa Shirikisho la soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino, amefunguliwa jalada la uchunguzi kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo rushwa.

Rais wa Shirikisho la soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino

Kwa mujibu wa sheria za nchi ya Uswis, Rais wa FIFA ni miongoni mwa viongozi wenye kinga, hivyo wanatakiwa kuombewa kuondolewa kinga ili wachunguzwe na tayari mwendesha mashtaka Mkuu wa Serikali ya Uswis ameshaomba ruhusa kwa Infantino pamoja na mtuhumiwa mwingine ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Uswis aliyejiuzulu Michael Lauber.

Uchunguzi wa tuhuma za rushwa ndani ya FIFA uliofanywa mwaka 2015 na kupelekea kumpa nafasi Gianni Infantino Februari 26, 2016 ya kuwa Rais wa FIFA, inaelezwa katika uchunguzi huo Infantino alitengeneza mazingira na kufanya uongo hivyo kunufaika kwa kuwa Rais wa FIFA.

Mwanasheria Mkuu wa Uswis aliyejiuzulu Michael Lauber

Baada ya kuwepo kwa malalamiko mengi juu ya hilo, uchunguzi umeanzishwa upya dhidi ya Infantino, Mwanasheria Mkuu aliyejiuzulu Michael Lauber pamoja na Mwendesha mashtaka wa Zürich Rinaldo Arnold.

Tuhumu kubwa kwa watu hao watatu ni kufanya mikutano ya siri kati yao, wakati ambao uchunguzi unaendelea mwaka 2015, ambapo walalamikaji wanaeleza kuwa ilimnufaisha Infantino.

Mwendesha mashtaka wa Zürich Rinaldo Arnold naye anadaiwa kumsaidia kwa kiasi kikubwa Infantino, ambaye anatoka naye eneo moja na wamekuwa pamoja tangu utotoni.

Mwendesha mashtaka wa Zürich Rinaldo Arnold

Mwaka 2015 FIFA ilikumbwa na kashfa kubwa ya rushwa, ambapo ilimlazimu aliyekuwa Rais wa FIFA wakati huo Sepp Blatter kujiuzulu na baadaye kufungiwa kutojihusisha na soka kwa miaka nane.