Jumatano , 18th Jul , 2018

Kuelekea mechi za robo fainali ya michuano ya Spri Bball Kings zitakazofanyika jumamosi Julai 22, 2018 kwenye uwanja wa ndani wa taifa, hii ni moja ya mechi zenye mvuto wa aina yake kutokana na uwezo wa timu hizo kwenye kuzuia na kushambulia.

Timu ya Water Institute

Kupitia takwimu za michezo ya hatua ya 16 bora, Water Institute ndio timu ya pili kwa kuiba mipira mingi kutoka kwa wapinzani wakiwa wameiba mipira 20 kwenye mechi yao dhidi ya Raptors. Wanazidiwa na St. Joseph ambao waliiba mipira 22 kwenye mchezo wao na Air Wing.

Water Institute walishinda kwa vikapu 77 dhidi ya 66 vya Raptors. Kitu kikubwa katika mchezo huo Water Institute walitokea nyuma katika quarter ya tatu ambapo walikuwa na vikapu 28 dhidi ya 40 vya Raptors kabla ya kupindua matokeo kwenye quarter ya 4 na kushinda.

Wakiwa na uwezo mkubwa wa kuzuia Water Institute kwenye robo fainali watakutana na Flying Dribbleres  ambayo kwenye mechi za hatua ya 16 bora ndio ilikuwa timu iliyoshambulia zaidi huku nyota wake Baraka Mopele akifunga pointi 36 kati ya 87 walivyofunga dhidi ya 63 vya Ukonga Hitmen.

Mechi zote 4 za robo fainali zitachezwa kwenye uwanja wa ndani wa taifa kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 2:00 usiku. Timu 4 zitakazoshinda zitaingia nusu fainali kisha mbil;i kwenda fainali na kumsaka bingwa atakayeondoka na milioni 10 huku mshindi wa pili akichukua milioni 3 na MVP milioni 2.