Vita ya Manara na Zakazakazi kuelekea ASFC

Jumanne , 30th Jun , 2020

Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara, Simba SC wanatarajia kukutana na Azam FC kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Azam Sports Federation Cup (ASFC).

Haji Manara na Zakazakazi

Kuelekea mchezo huo, kumekuwepo na vita ya maneno kati ya Mkuu wa Idara ya Habari ya Azam FC, Zakaria Thabit 'Zakazakazi' na mwenzake wa Simba, Haji Manara, hii ni mara baada ya Simba kutangazwa kuwa bingwa.

Kwa upande wa Haji Manara, amenukuliwa akikereka na kauli ya Zakazakazi ambaye ameutafsiri ubingwa wa Simba kuwa haukuwa wa ushindani kwani makosa mengi ya maamuzi yametokea kwenye msimu huu.

Manara amesema, "nimemsikia msemaji wa Azam akisema ubingwa wetu wa kupewa, nawaheshimu sana Azam lakini wasisingizie tulibebwa, hii ni kukosa heshima yetu. Nimshukuru sana kocha wa Yanga, Luc Eymael amekuwa mtu wa kwanza kumpigia simu kocha Sven kumpongeza kwa kutwaa ubingwa pia GSM wamenipigia simu na kutupongeza pia".

''Wakati wanafungwa na Kagera Sugar sisi tulikuwepo huko?, wakati wanatoka sare kwani sisi tulikuwepo, wanapaswa kutuheshimu mabingwa mara tatu mfululizo", ameongeza Manara alipokuwa akihojiwa.

Naye Zakazakazi amemjibu Manara katika mtandao wa Instagram akisema, "huhusu kuwaponda mabingwa yawezekana ulihadithiwa na mtu ambaye hakuelewa nilichokisema, au ulisikia ukiwa kwenye mhemko mkubwa sana. Sikuwaponda mabingwa na wala sikuwagusa popote, zaidi ya kuwapongeza. Niliwapongeza mapema, mara tu baada ya mchezo tena kupitia vyombo vya habari na kupitia akaunti binafsi ya Instagram".

"Lakini baada ya pongezi, nilitoa wito kwa waamuzi msimu ujao wafanye vizuri zaidi ya msimu huu ili bingwa asichafuliwe ubingwa wake kwa makosa yao. Msimu huu ulikuwa moja ya misimu ambayo waamuzi wamefanya vibaya sana kiasi cha kamati ya waamuzi ya TFF kuvunjwa katikati ya msimu", ameongeza.

Pia Zakazakazi amesema kuwa kipimo cha ubingwa siyo lazima iwe mabao ya kinara wa orodha ya wafungaji bora, msimu wa 2011/12, Simba walikuwa mabingwa, na John Bocco wa Azam FC alikuwa na mabao 19 na kinara wa mabao wa Simba alikuwa Emmanuel Okwi aliyefunga mabao 12, mabao mawili kati ya hayo, aliyafunga siku  ya mwisho ya msimu, katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Yanga.