Jumamosi , 29th Aug , 2020

Usiku wa hii leo majira ya saa 12:30 jioni saa za Afrika Mashariki kutakuwa ufunguzi wa pazia la Ligi Kuu soka nchini Uingereza EPL kwa mechi ya ngao ya jamii kati ya mabingwa wa EPL Liverpool mabingwa wa FA, Arsenal 'The Gunners.

Mchezo wa Kombe la ngao ya jamii

Mchezo wa leo unatarajiwa kuwa ni wa 229 kuwakutanisha Arsenal na Liverpool. Majogoo Liverpool wako mbele kwa ushindi wa michezo 10 ambapo wana jumla ya ushindi wa michezo 89 kati ya michezo yote ilhali Arsenal wameshinda michezo 79 na jumla ya michezo 61 ya wababe hao walitoshana nguvu kwa kuisha kwa suluhu.

Wababe hawa wanaingia mchezoni hii leo huku wakiendelea na zoezi la kuimarisha vikosi vyao ambapo katika mkutano wa waandishi wa habari hapo jana kocha wa Liverpool raia wa Ujerumani Jurgen Klopp alinukuliwa akisema

"Idadi ya wachezaji bora katika kikosi chetu ni ya kuridhisha sana, tuna kikosi kipana zaidi wakati huu huku kikichagizwa na uwepo wa damu changa kikosini, idadi ya kikosi chetu ni ya kuridhisha mno", amesema Klopp.

Aidha Klopp ameeleza kufurahishwa na kikosi chao huku akidai wanategemea pia kuboresha kikosi kwa kuimarisha viwango vya wachezaji walionao sasa.

Kwa upande wa washika mitutu Arsenal chini ya kocha wake Mikel Arteta anaonesha dhamira ya dhati ya kuitengeneza Arsenal mpya na ya ushindani baada ya kufanya sajili za wachezaji wenye ubunifu, uzoefu na wa daraja la juu akiwemo Willian.

Arsenal pia imemsainisha Mchezaji kijana mwenye miaka 22 katika nafasi ya kiungo mkabaji Gabriel Magalhaes anaetarajiwa kutua klabuni humo akitokea Lille ya Ufaransa akiwa ndiye mchezaji anayetazamwa zaidi katika ubora wa nafasi hiyo barani Ulaya atakayeungana na William Saliba.

Katika mechi 5 za hivi karibuni za vilabu hivyo takwimu zinaonesha Liverpool ameshinda Michezo mitatu, suluhu moja na kufunga mchezo mmoja. Wakati Asenal wameshinda michezo minne na kufungwa mchezo mmoja.