Jumanne , 2nd Jun , 2020

Kuelekea kurejea kwa Ligi Kuu Tanzania bara Juni 13, Bodi ya Ligi Tanzania TPBL imesema imeshawalipa waamuzi wote kwa kushirikiana na TFF na kwamba haina deni lolote hivi sasa.

Mwamuzi wa VPL na kocha wa Yanga, Luc Eymael

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, TPBL imesema kuwa imeshawalipa jumla ya TZS 555,661,400 waamuzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili kwa msimu wa 2019/20.

Hiyo imekuja kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa waamuzi wanaolalamikia kutolipwa stahiki zao kunakopelekea maisha kuwa magumu hasa katika kipindi hiki cha COVID-19.

Jitihada zilizofanywa na TPBL na Shirikisho la Soka Tanzania TFF zitasaidia kuweka mazingira sawa ya kimchezo na kuondoa au kupunguza vishawishi vya rushwa kwa waamuzi, kwani kumekuwepo na malalamiko ya baadhi ya waamuzi kushawishika kuingia katika rushwa kutokana na kutolipwa stahiki zao kwa wakati.

Ligi inatarajia kuanza Juni 13 kwa michezo miwili, Mwadui FC dhidi ya Yanga na Coastal Union dhidi ya Namungo FC huku ikisisitiza kuwa katika ligi zote tatu ni lazima mabingwa wapatikane.