Jumanne , 3rd Nov , 2020

Mtendaji mkuu wa bodi ya ligi Almas Kasongo ametangaza kuwa kuelekea mchezo wa watani wa jadi kati ya Simba na Yanga wamejipanga kutumia waamuzi sita watakaochezesha mchezo huo.

Mtendaji mkuu wa TPLB, Almas Kasongo (Katikati), na Mkurugenzi wa Michezo kutoka Wizarani Yusuph Singo(Wa kwanza kulia) wakizungumza na Waandishi wa Habari.

Kasongo amesema waamuzi wawili wanatarajiwa kuwa nyuma ya magoli ya pande zote mbili, mmoja wa atakuwa mwamuzi wa kati na wawili wa pembeni yaani vibendera na mmoja mwamuzi wa mezani.

Licha ya kwamba waamuzi hao bado hawajawekwa hadharani lakini mtendaji mkuu wa TPLB Almas Kasongo amesema kwamba muda wowote watatangaza majina yao.

Vilevile bodi ya ligi imetangaza rasmi kwamba mchezo huo utachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya marekebisho kukamilika.

Mchezo huo utachezwa Novemba 7 mwaka huu majira ya saa 10 jioni ambapo miamba hiyo ya mpira nchini itakapoumana kusaka alama tatu muhimu na heshima.