Jumapili , 8th Jul , 2018

Hatimaye timu 8 zitakazochuana katika hatua ya robo fainali ya michuano ya mpira wa Kikapu nchini Sprite Bball Kings, zimepatikana baada ya mechi za hatua ya 16 bora kukamilika jioni ya leo.

Baadhi ya wachezaji wa timu ya Mchenga Bball Kings na Oysterbay wakati wa mchezo wao leo.

Mabingwa watetezi Mchenga Bball Stars, wakiwa na nia ya kutetea ubingwa wao, walijihakikishia nafasi ya robo fainali mapema tu leo walipowalaza Oysterbay vikapu 117 kwa 56. 

Mchenga leo wameungana na timu za Temeke Heroes ambayo imewatoa Stylers kwa vikapu 76 dhidi ya 58, Team Kiza ambayo imewanyoosha Ukonga Warriors kwa vikapu 66 dhidi ya 56 pamoja na Water Institute ambao wamewalaza Raptors kwa pointi 77 kwa 66.

Baada ya timu hizo kujulikana, droo ya robo fainali itachezeshwa kesho na kuonekana 'Live' kwenye kipindi cha 5Sports cha East Africa Television na kusikika kupitia The Cruise ya East Africa Radio.

Ikumbukwe kuwa bingwa wa michuano hii inayoandaliwa na East Africa Television LTD na kudhaminiwa na kinywaji baridi cha Sprite, atajinyakulia kitita cha shilingi milioni 10 huku mshindi wa pili akipokea milioni 3 na MVP atachukua milioni 2.