Jumapili , 16th Dec , 2018

Inaelezwa kuwa wachezaji wa Simba wameahidiwa bonasi kubwa zaidi ya pesa na uongozi wa klabu endapo watafanikiwa kuwaondoa Nkana Red Devils kwa kupata ushindi katika mchezo wa marudiano Jijini Dar es salaam.

Simba

Pia katika hatua nyingine, kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems amewapatia uongozi wa Simba chini ya mwekezaji Mohamed Dewji 'MO', muongozo wa kutoa pesa kwa wachezaji kama bonasi kila wanaposhinda au kusuluhu lakini pesa hizo zitatofautiana na uzito wa mashindano husika.

Mastaa hao wa Simba wanaposhinda kila mechi ya ligi kuu hupata pesa, ila kwa mechi za kimataifa mzigo ndio huwa mkubwa zaidi kuliko mechi zamichuano ya nyumbani.

Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, bonasi wanayowapa wachezaji wao ni pesa ya kutosha na kusisitiza kuwa pesa hiyo itazidi kuongezeka kadri timu itavyozidi kusonga mbele katika mashindano hayo ya kimataifa.

Simba imepoteza mchezo wa mkondo wa kwanza kwa mabao 2-1 dhidi ya Nkana Red Devils nchini Zambia, ambapo inatarajia kurejea leo nchini tayari kwa maandalizi ya mchezo wa marudio utaopigwa wiki ijayo Jijini Dar es salaam.

Inahitaji kupata ushindi wa bao 1-0 au zaidi ili iweze kuwaondoa Nkana na kusonga mbele katika hatua inayofuata ya makundi ya michuano hiyo mikubwa zaidi barani Afrika kwa ngazi ya klabu.