Jumatatu , 26th Nov , 2018

Kuelekea ufunguzi wa msimu wa michuano ya vilabu barani Afrika hapo kesho, kocha wa kikosi cha Mtibwa Sugar, Zuber Katwila amesema kuwa ana imani kubwa na kikosi chake kuibuka na ushindi dhidi ya Northern Dynamo ya Shelisheli licha ya kutokuwa na wachezaji wa kigeni.

Katika mchezo huo utakaopigwa katika uwanja wa Chamazi jijini Dar es salaam, Mtibwa Sugar inatarajia kucheza mchezo wake wa kwanza wa kimataifa wa kombe la shirikisho kwa mara ya kwanza tangu takribani miaka 15 iliyopita.

Akizungumza na www.eatv.tv kuelekea mchezo huo, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila amesema, "wachezaji wanatambua kazi yao na wamepata mafunzo makini kwa kuwa maandalizi tuliyaanza mapema hatuna mashaka katika hilo licha ya kutowafahamu vizuri wapinzani wetu na kutokuwa na mchezaji wa kigeni".

"Wachezaji wa kigeni si kitu, sisemi kuwa hawana uwezo ila mimi nawaamini wachezaji wangu kutokana na uzoefu walionao utawasaidia kwa kuwa tumecheza michezo mingi ya Ligi Kuu pamoja na ile ya kirafiki hali inayonipa imani kwamba tutafanikiwa kuipeperusha vema bendera ya nchi, mashabiki wajitokeze kutupa sapoti," amesema.

Timu nyingine itakayoiwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa ni Simba ambayo itacheza mchezo wake wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Mbabane Swallowa ya Swartzland, mchezo ambao utachezwa Jumatano katika uwanja wa taifa.