Wachezaji wa Man United wakishangilia bao.
Ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Fullham ndio umewapa jeuri Man United ya kukaa katika nafasi ya 4 kwa muda wakiwa na alama 51, ikiwa ni moja zaidi ya Chelsea ambayo kesho inacheza na Manchester City.
Katika ushindi wa leo, wachezaji wawili wa Man United raia wa Ufaransa, Paul Pogba na Anthony Martial, ndio waliofunga mabao hayo matatu huku kila mmoja akiweka rekodi yake.
Kwa upande wa Paul Pogba yeye amefunga mabao 7 mpaka sasa akiwa chini ya kocha Ole Gunnar Solskjær, hivyo kufanya sasa asilimia 38% ya mabao yake 23 aliyofunga kwenye Ligi kuu ya England, kuwa amefunga chini ya kocha huyo ambaye ameiongoza Man United katika mechi 11 mpaka sasa bila kufungwa.

Kwa upande wa Anthony Martial yeye amehusika katika mabao 50 ya Man United kwenye ligi kuu ya England tangu aliposajiliwa klabuni hapo. Amefunga mabao 33 na Assist 17.

Kwa upande wa Manchester United yenyewe mpaka sasa imekuwa klabu iliyofunga mabao mengi zaidi ya penalti msimu huu katika ligi hiyo. Imefunga mabao 7 na hiyo ni baada ya bao la penalti la Pogba ambalo lilikuwa la pili kwake, kwenye mchezo wa leo na la tatu kwa Man United.





