Ijumaa , 15th Oct , 2021

Kocha wa Klabu ya Simba, Didier Gomes Da Rosa ameweka wazi kuwa malengo yao makubwa msimu huu ni kufika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya mabingwa Afrika.

Didier Gomes Da Rosa

Gomes ameyasema hayo muda mchache baada ya mazoezi ya mwisho ambayo ni ya maandalizi kabla ya kuianza safari ya kuelekea nchini Botswana ambapo watacheza mchezo wao wa kwanza wa michuano ya Ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy  utakaochezwa siku ya Jumapili ya Oktoba 17, 2021.

''Kwanza mjue malengo yetu makubwa ni kufanya vyema msimu huu wa Ligi ya mabingwa, na tumedhamiria kutinga nusu fainali, tunahitaji kuwa bora zaidi kuliko msimu uliopita, tumedhihirisha hilo mara ya mwisho tulitinga robo fainali, ili tufanikiwe tunahitaji kuwa na nidhamu kubwa katika kila mchezo tukianzia dhidi ya Galax Jwaneng  huko Botswana''Didier Gomes Da Rosa.

Katika hatua nyingine kocha huyo amesema amefatilia mechi ya mwisho ya wapinzani wao wa siku ya Jumapili ambapo amebaini wapo imara kwenye mpira wa juu, na wanakaba vizuri hivyo ameandaa mpango wa kushambulia kwa njia mbalimbali ili wafanikiwe malengo yao.

Kwa upande wa nahodha wa Simba, John Bocco amesema wamefanya mazoezi mazuri na wamejipanga kupata ushindi huku akisisitiza kuwa msimu huu utakuwa mgumu kwani vilabu vitakuwa vimejiandaa kikamilifu ili zipate matokeo.

Wekundu wa msimbazi walitinga robo fainali ya michuano hiyo msimu uliopita na walikaribia kucheza nusu fainali lakini waliondolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini kwa kunyukwa bao 4-3 katika michezo miwili.