Jumapili , 7th Jan , 2018

Klabu ya soka ya Yanga SC leo itashuka dimbani kucheza mechi yake ya nne ya Kundi B kwenye Kombe la Mapinduzi dhidi ya Zimamoto huku ikitafuta ushindi ili kuifikia Singida United.

Yanga tayari imeshafuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kushinda mechi zake tatu za mwanzo, lakini itakuwa inasaka alama tatu ili kujiweka kwenye maZingira mazuri ya kumaliza ikiwa kinara a Kundi B.

Kundi B kwasasa linaongozwa na Singida United yenye pointi 12 baada ya mechi nne hivyo endapo Yanga leo itashinda itafikisha alama 12 na kusubiri mechi ya mwisho ambapo timu hizo zitakutana kesho kuamua nani ataongoza kundi.

Baada ya mchezo wa leo, hatua ya makundi itakamilika kesho Januari 8 kwa mechi mbili kupigwa ambapo Simba SC na URA ya Uganda zitacheza kufunga mechi za kundi A huku Yanga SC na Singida United  zitafunga michezo ya kundi B.

Nusu fainali zitacheza Januari 10 na fainali zitachezwa Januari 13. Kwa upande wa kundi A tayari mabingwa watetezi Azam FC wameshatangulia nusu fainali hivyo mechi ya Simba SC na URA itaamua nani aungane na Azam FC.