Yanga na Wajelajela kumalizana J'mosi hii

Friday , 21st Apr , 2017

Mchezo wa Robo Fainali ya Nne ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara kati ya Young Africans na Tanzania Prisons FC utafanyika kesho Aprili 22, 2017  kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo utatoa mshindi ambaye ataungana na timu nyingine tatu ambazo tayari zimefuzu kwa hatua ya Nusu Fainali ambazo ni Mbao FC, Simba SC na Azam FC.

Jumapili Aprili 23, mwaka huu kutakuwa na droo ya wazi kwa timu nne zitakazokuwa zimefuzu kwa hatua ya Nusu Fainali

Azam FC ilikata tiketi ya kucheza Nusu Fainali baada ya kuifunga Ndanda FC mabao 3-1, kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam Aprili 5, 2017 ikitanguliwa na Mbao iliyoishinda Kagera Sugar mabao 2-1 katika mchezo ulifanyika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera Machi 18, 2017.

Machi 19, mwaka huu Simba iliwatoa Madini ya Arusha kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na kufuzu hatua hiyo

Tarehe za michezo hiyo ya nusu fainali pamoja na fainali bado hazijawekwa hadharani.

Bingwa wa michuano hii ambayo msimu huu ilishirikisha timu 86 atazawadiwa Sh. 50 milioni na kupata tiketi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho - CAF.