Alhamisi , 2nd Jun , 2016

Wakati Uongozi wa Yanga ukianza kusaka na kukamata baadhi ya wanachama wanaowahisi kutaka kufanya hujuma ya uchaguzi mkuu wa klabu hiyo na huku tayari baadhi yao wakiadhibiwa kutokana na tuhuma hizo, TFF wao watatoa tamko lao Juni 8 mwaka huu.

Baadhi ya wanachama wa Yanga katika moja ya mikutano ya wanachama wa timu hiyo.

Uongozi wa klabu ya Yanga umemfuta uanachama mwanachama mmoja aliyesikika akipanga njama za kuhujumu uchaguzi wa klabu hiyo na kuwapeleka wengine tisa katika kamati ya maadili ya timu hiyo.

Mkuu wa idara ya habari ya timu hiyo Jerry Muro amesema klabu hiyo inafanya kila kitu kwa mujibu wa sheria na katiba yao na kila mtu anayetaka kufanya hujuma atagundulika.

Jerry amesema kwakuanza kukabiliana na watu hao Uongozi wake ulileta mpelelezi kutoka nje ya nchi kufanya uchunguzi juu ya watu hao na akanasa mbinu hizo chafu hadi ushahidi wa sauti.

Katika sauti hizo ambazo zilichezwa mbele ya wanahabari zilisikika sauti ambazo Jerry amethibitisha ni za baadhi ya wanachama wa klabu hiyo [Yanga] wakipanga njama hizo kwa kushirikiana na watu wa TFF na BMT ili kuvuruga uchaguzi huo na kukata baadhi ya majina ya watu wasioweataka kwa maslahi yao.

Aidha Jerry amesema wazi kuwa hiyo ndiyo sababu hawana imani na TFF kuendesha uchaguzi wao na akasistiza Yanga itafanya yenyewe uchaguzi wake, tu kwa kusimamiwa na TFF na sivinginevyo.

Baada ya uongozi wa Yanga kupitia kwa Jerry kuwasikilizisha Waandishi wa Habari na wanachama waliokuwapo katika mkutano wa hii leo sauti hizo, Uongozi huo ukatangaza kumfuta uanachama, mwanachama ambaye sauti yake imevuma zaidi kwenye rekodi hiyo, akijulikana kwa jina moja la Msumi ambaye ataitwa Kamati ya Maadili kujieleza.

Na pia uongozi wa timu hiyo umewafuta uanachama wanachama wale wote ambao nao sauti zao zimo kwenye clip hiyo.

Pamoja na hayo, Uongozi wa klabu ya Yanga imemuagiza Afisa Habari wa klabu, Jerry Muro kupeleka sauti hizo Jeshi la Polisi Tanzania na taasisi ya kupinga na kupambana na rushwa nchini Tanzania TAKUKURU kwa ajili ya uchunguzi zaidi na baada ay hapo aendelee kutoa taarifa kila kinachoendelea kwa kila hatua.

Kwa upande mwingine uongozi wa klabu hiyo unataraji kuwapeleka wabachama wake tisa katika kamati ya maadili ya timu hiyo kutokana na kitendo cha utovu wa nidhamu cha kwenda kuchukuwa fomu za kugombea nafasi za uongozi wa klabu hiyo katika ofisi za shirikisho la soka nchini Tanzania TFF ambao ni wasimamizi tu na si wenye uchaguzi huo.

Zoezi la utoaji Fomu za kugombea nafasi zote za uongozi wa timu hiyo katika uchaguzi wa klabu hiyo ambao utafanyika Juni 11 mwaka huu tofauti na ule wa TFF uliopangwa kufanyika Juni 25 mwaka huu zimeanza hii leo Juni 02 nakumalizika jioni ya kesho Juni 03.

Baadhi ya wanachama ambao wamekumbana na rungu hilo ambao tayari walishajitokeza kuchukuwa fomu za kuwania uongozi wa klabu hiyo ni pamoja na Aaron Nyanda na Titus Osoro wanaowania nafasi ya makamu mwenyekiti kwa mujibu wa katiba ya mwaka 2010 inayotambulika serikalini hadi sasa.

Wengine ni Paschal Laizer, Edgar Chibula, Mohammed Mattaka, Mchafu Ahmed Chakoma, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ Omari Said kutoka Zanzibar.

Wakati huo huo shirikisho la soka nchini Tanzani linataraji kutoa tamko rasmi juu ya uchaguzi wa klabu hiyo ifikapo Juni 8 mwaka huu na wako makoni na kimsingi TFF inafuatilia kwa karibu mwenendo mzima wa mchakato na taarifa zote zitatolewa na TFF kupitia wasemaji wake na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ambaye ni Wakili Msomi, Alloyce Komba.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linapenda kuwafagamisha wanachama wa Young Africans na familia ya mpira kwa ujumla kuwa mchakato wa uchaguzi wa Klabu ya Young Africans uko pale pale na wanatakiwa kuwa watuli na kusubiri nini TFF watatamka kuhusu hatma ya uchaguzi huo.