Jumamosi , 8th Aug , 2020

Klabu ya Yanga maarufu kama wababe wa mitaa ya Twiga na Jangwani mchana wa leo Agosti 8, 2020,  kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii imesema kuwa imesikitishwa na kitendo cha Klabu ya Simba kumsajili Bernard Morrison.

Bernard Morrison

Katika barua ya wazi kwa umma uongozi wa Yanga umesema kuwa, unafuatilia kwa karibu suala hilo na pindi itakapobainika kuwa Simba imemsainisha Morisson basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa ili iwe mfano kwa vilabu vingine nchini.

Utata wa usajili wa kiungo huyu mshambuliaji machachari Bernard Morisson ama BM33 mpanda mipira, limekuwa likifukuta chinichini kwani upande wa Bernard Morrison haujaafiki mkataba wa miaka miwili unaoelezwa kuwepo kati yake na Yanga na kudai kuwa mkataba uliokuwepo baina yao ni wa miezi 6 na ulikwisha.

Suala hili lilifika hadi Shirikisho la Mpira wa miguu nchini ambapo Yanga walidai Morrison ni mchezaji wao, wakati huohuo Morrison anadai kuwa mkataba unaoonekana ni batili kwani sahihi iliyopo imeghushiwa.