Yanga inayoiwakilisha Tanzania katika michuano hiyo, imeshusha kikosi chake kamili hii leo licha ya kumkosa Haruna Niyonzima na kuanza mchezo kwa kasi lakini ilijikuta ikianza kufungwa bao dakika ya 11, lililofungwa na Amri Gamal aliyeunganisha kwa kichwa kros iliyotokana na mpira wa adhabu.
Bao la Yanga limepatikana dakika ya 19 baada ya mchezaji Ahmed Hegazy wa Al Ahly kujifunga katika harakati za kuokoa mpira uliopigwa na kiungo wa Yanga Boubacar Issouf kutoka winga ya kushoto na kufanya hadi kipindi cha kwanza kinamalizika matokeo kuwa 1-1.
Katika kipindi cha pili, Yanga walirudi kwa nguvu lakini Al Ahly walionekana kumaliza nguvu za Yanga kwa kumiliki mpira muda mrefu huku wakifanya mashambulizi ya kushitukiza, jambo ambalo lililazimu benchi la ufundi la Yanga Kufanya mabadiliko.
Katika mabadiliko yaliyofanywa, walitoka Issouf Baoubacar na Amis Tambwe na nafasi zao kuchukuliwa na Geofrey Mwashiuya na Simon Msuva ambao kwa kiasi fulani walisaidia kuongeza kasi ya mchezo.
Kati ya dakika ya 70 na 75 kipa namba moja wa Yanga Ally Mustapha alipata dhoruba na kulazimika kutoka nje na nafasi yake kuchukuliwa na Deo Munisi.
Hadi mpira unakwisha Yanga 1 Al Ahly 1.
Matokeo haya yanaipa Yanga mtihani mzito katika mchezo wa marudiano kwani ili kufuzu hatua inayofuata inalazimika kushinda ugenini nchini Misri au kutoka sare ya kuanzia mabao 2-2.
Kesho wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Azam FC wanashuka katika dimba la Chamazi kuikabili Esperance ya Tunisia.