Yanga yaizamisha Majimaji FC

Jumatano , 14th Feb , 2018

Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara klabu ya Yanga, imeibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Majimaji FC ya Songea kwenye mchezo wa ligi kuu soka Tanzania Bara uliomalizika jioni hii.

Yanga ambayo imeshinda mchezo wake wa sita mfululizo imeendelea kupigania kutetea taji lake ambapo sasa imefikisha alama 37 nyuma ya Simba yenye alama 41 kwenye msimamo wa ligi.

Mabao ya Yanga leo yamefungwa na nyota wake Obrey Chirwa, Emmanuel Martin na Tshishimbi Kabamba aliyefunga mawili na kuifanya sasa timu hiyo ikamilishe ushindi wa tano katika michezo ya ligi kuu ya hivi karibuni na sita ukijumlisha na michuano ya kimataifa.

Baada ya ushindi huu Yanga inatarajiwa kuondoka nchini siku ya Jumapili kuelekea nchini Shelisheli kwaajili ya mchezo wa marudiano utakaopigwa Februari 21 dhidi ya wapinzani wao St. Louis.

Baada ya mchezo wa leo ambao ulikuwa ni wa kiporo kesho vinara Simba wanatarajiwa kushuka kwenye dimba la Kambarage Shinyanga kucheza na Mwadui FC.