Alhamisi , 22nd Apr , 2021

Kaimu khatibu mkuu wa klabu ya Yanga, Haji Mfikirwa amesema wana malengo makubwa ya kuikuza Yanga kwenye Nyanja zote baada ya kusaini mkataba wa ushirikiano na klabu ya Raja Club Athletic ya nchini Morocco siku ya jana Aprili 21, 2021.

Kaimu Khatibu Mkuu wa Yanga, Haji Mfikirwa (kulia) akisaini mkataba wa ushirikiano na moja ya kiongozi wa klabu ya Raja Casabalanca.

Akiongea baada ya zoezi la utiaji saini, Mfikirwa amesema: 

“Sisi makubaliano yetu yanalenga katika malengo mbali mbali hasa katika timu yenyewe na klabu kiujumla. Mambo ya utawala na usimamizi wa rasirimali, mambo ya mabadiliko ya teknolijia na kupeana uzoefu wa kiuongozi na masuala ya mustakhabali mzima wa mpira”.

“Kwahiyo tunazungumzia uwezekano wa kubadilishana wachezaji na kuwapa nafasi vijana wapate nafasi kubwa zaidi, lakini pia tumegusia masuala ya wao kupata fursa zinazopatikana Tanzania kwa maana ya wachezaji waweze kwenda mbele zaidi”.

“Lakini pia tumegusia kushirikiana kwenye masuala mazima ya kusaka udhamini, kwahiyo ni eneo pana linaloakisi dhamira yetu nzima ya mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu, kwasababu unapofanya mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu nia kubwa ni kuweza kufungua wigo mpana”.

“Pia tutashirikiana na tutabadilishana uzoefu kwa namna gani tutapata faida ya kuwa na mashabiki wengi katika kuimarisha vilabu vyetu”.

(Viongozi wa klabu ya Raja Athletic Club Casablanca wakionesha mkataba na moja ya kiongozi wa Yanga)

Yanga imekuwa timu ya pili kusaini kandarasi hiyo na mabingwa hao wa kombe la shirikisho Afrika kwa msimu wa 2018 iliyolenga maendeleo ya klabu baada ya Namungo kusaini kandarasi hiyo.