Ijumaa , 6th Sep , 2019

Uongozi wa klabu ya Yanga umepeleka malalamiko kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ukipinga uamuzi wa Bodi ya Ligi kumfungia kocha Mwinyi Zahera.

Fredrick Mwakalebela (kushoto) akiwa na moja ya kiongozi wa klabu katika mkutano na wanahabari

Mwanzoni mwa wiki hii TFF ilitoa adhabu kwa kocha Zahera ya kumfungia mechi tatu kutokana na shutuma za upendeleo alizotoa kwa Bodi hiyo baada ya mchezo wa kwanza wa ligi kati ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela amesema kuwa adhabu ya kumfungia kocha mechi tatu ni kubwa na kwamba pengine faini ingetosha kumrekebisha.

"Unapomfungia kocha mechi tatu kwa nini usimpe faini tu aendelee kufundisha timu?. Tumeshaiandikia barua Wizara kulalamikia haya madhaifu na tunasubiri majibu", amesema Mwakalebela.

Aidha kiongozi huyo amefafanua kuwa klabu hiyo haitovaa jezi zenye nembo nyekundu ya mdhamini mkuu wa Ligi Kuu Tanzania bara msimu huu kwa sababu hawana utamaduni wa kutumia rangi hiyo huku akitaja rangi za klabu hiyo kuwa ni njano na kijani.