Yanga yatimiza miaka 84, fahamu usichokijua

Jumatatu , 11th Feb , 2019

Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, kwa maana ya mwaka 1935, iliundwa klabu ya Yanga, ambayo wakati inaanzishwa ilikuwa ukijulikana kama 'Jangwani Boys'.

Klabu ya Yanga

Hiyo ilikuwa ni baada ya baadhi ya vijana waliokuwa wakikutana jioni katika mitaa ya Jangwani, kuamua kuanzisha klabu hiyo.
Licha ya kuwa ni klabu ya michezo, Yanga pia ilitajwa kwa kiasi kikubwa kuhusika katika harakati za ukombozi wa taifa, ambapo ilipelekea kupatikana kwa uhuru, mnamo mwaka 1961.

Mara ya kwanza kushinda ubingwa wa ligi kuu, ambapo ilikuwa ikijulikana kama ligi daraja la kwanza ni mwaka 1968 na mpaka sasa imeshinda ubingwa huo mara 27 na kuongoza katika listi ya klabu zilizoshinda mara nyingi zaidi ubingwa wa ligi.

Yanga pia imeshinda kombe la shirikisho mara nne, na mara ya mwisho kushinda ni msimu wa 2015/16.

Katika michuano ya vilabu ya Afrika Mashariki na Kati ( CECAFA Kagame Cup ) Simba imeshinda mara tano na mara ya mwisho ni mwaka 2012.

Pamoja na mafanikio makubwa katika soka la ndani na Afrika Mashariki na Kati, klabu ya Yanga mpaka sasa haijafanikiwa kufanya vizuri katika michuano mbalimbali ya vilabu barani Afrika, kwani imekuwa ikiishia katika hatua za makundi ya michuano hiyo, huku historia kubwa iliyo nayo ni kufika robo fainali ya michuano ya kombe la washindi la CAF mwaka 1995.

Changamoto nyingine licha ya kuwa na umri mkubwa mpaka sasa, Klabu ya Yanga imeshindwa kuwa na uwezo mkubwa wa kujitegemea kama klabu, kwani haina uwanja wa kisasa wa mazoezi na wa mechi, hosteli za wachezaji na kituo cha kisasa cha kukuzia vijana.