Ijumaa , 23rd Nov , 2018

Kocha mkuu wa kikosi cha Yanga, Mwinyi Zahera amefichua ukweli juu ya sababu ya kutomchezesha nyota wa timu hiyo, Ibrahim Ajib katika mchezo dhidi ya Mwadui FC licha ya kuonekana kuwa fiti.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera

Katika mchezo huo wa ligi kuu Tanzania bara uliochezwa mjini Shinyanga Alhamisi ya Novemba 22, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1. Mabao yaliyofungwa na Heritier Makambo na Mrisho Ngassa.

Akizungumza juu ya kutomchezesha Ajibu katika mchezo huo, kocha Mwinyi Zahera amesema, " wakati mimi nasafiri kwenda kwenye timu ya taifa nchini Congo, nilimuachia kocha programu ya mazoezi na kila siku alikuwa akinipatia ripoti ya mchezaji gani alikuja na nani hakuja. Katika siku 10, Ibrahim Ajibu alikuja kwenye mazoezi siku nne," amesema Zahera.

"Tulicheza mechi tatu za kirafiki na katika mechi mbili Ajibu hakucheza, hakuonekana, na mimi nikasema wakati narudi na anakuja kufanya mazoezi, siwezi kumchezesha mchezaji ambaye hafanyi mazoezi. Napenda hata kama nikifungwa na wachezaji wenye nidhamu " ameongeza kocha huyo.

Ajibu ameikosa mechi hiyo ambayo ilikuwa ni ya kwanza kwa Yanga kucheza mechi nje ya jiji la Dar es Salaam kwa katika huu kutokana na kushindwa kuhudhuria programu ya siku nne ya mazoezi, ambayo kocha amesema hakuona haja ya kumpanga.

Baada ya mchezo huo, sasa Yanga inashika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kwa jumla ya alama 29 katika michezo yake 11 iliyocheza huku nafasi ya kwanza ikiongozwa na Azam FC. Mpinzani wake wa karibu, Simba imeshuka hadi nafasi ya tatu kwa alama 26.